SAFARI ZA TRENI ZA ABIRIA KUTOKA DAR KUELEKEA BARA ZAREJEA RASMI

posted in: Press Release | 0

 

TAARIFA KWA UMMA

KUREJEA KWA USAFIRI WA TRENI ZA ABIRIA

Kampuni ya Reli Tanzania(TRL) inautangazia umma kurejea kwa safari zake za treni za abiria zitakazoanzia kituo cha Dar es Salaam kuelekea bara siku ya Ijumaa tarehe 02/03/2018. Safari za treni zilisitishwa kwa muda tangu tarehe 11/01/2018 baada ya mafuriko kuharibu miundombinu ya reli katika eneo la Kilosa na Gulwe.

Uamuzi huu wa kurudisha huduma kuanzia hapa Dar Es Salaam umetolewa na Kampuni baada ya kufanya tathmini ya  ukarabati uliofanyika  kwa kipande hicho cha njia ya reli kati ya Kilosa na Gulwe uliochukua takribani mwezi mmoja kukamilika. Mara baada ya kuona kwamba njia inaweza kutumika kwa  marekebisho hayo ilibidi kampuni ianze huduma katika eneo hilo kwa kupitisha  treni za mizigo ambapo zilianza siku ya tarehe 12/02/2018 mara baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mh. Prof. Makame M. Mbarawa kufungua rasmi njia hiyo.

Tayari treni za mizigo zaidi ya thelathini  zimeshapita katika eneo hilo bila ya tatizo lolote kujitokeza.Hali hiyo inadhihirisha kuwa njia ya reli  katika eneo hilo ni salama kwa kupitisha abiria zetu.

Uongozi wa TRL umejiridhisha na hali ya kiusalama katika eneo hilo kutokana na hatua za kiusalama zilizochukuliwa wakati wa ukarabati na hata baada ya ukarabati wa eneo hilo  wa njia hiyo ya reli.

Treni yetu  ya kwanza inatarajia kuanza safari zake  siku ya Ijumaa saa tisa Alasiri kutoka kituo cha Dar es Salaam kuelekea Morogoro, Dodoma,Tabora na  Kigoma. Treni hizo zitaendelea na ratiba zake kamazilivyokuwa hapo awali.

Aidha ile treni ya abiria ambayo inatarajiwa kuondokaleo katikakituo cha Dodoma kuelekea Tabora na Kigoma, treni hiyo itatoka Kigoma  tarehe 01 Machi,2018 na kuja moja kwa moja Dar es Salaam.

Kwa hali hiyo treni zetu zitaendelea kufuata ratiba zake za zamani kuanzia Dar essalaam. Tunazo huduma nne kwa wiki ambapo ile treni ya Deluxe ipo kila Alhamisi tu. Siku nyingine ni kila Jumanne, Ijumaa na Jumapili.

Kampuni ya Reli Tanzania inaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa abiria kutokana na kusitishwa kwa muda kwa huduma za usafiri wa treni za abiria na inawakaribisha tena kwenye safari za treni za abiria na mizigo.

IMETOLEWA NA:

Ofisi ya Uhusiano

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji

Kampuni ya Reli Tanzania

Dar es Salaam

Leave a Reply