KIPANDE CHA RELI KATI YA MOROGORO NA MAKUTOPORA KUGHARIMU ZAIDI YA TRILIONI 4!

posted in: Media, Press Release | 0

Leo mchana Septemba 29, 2017, Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Nchini (Rahco) imeingia mkataba na Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki kujenga kipande cha pili cha reli ya kisasa ya Standard gauge(SGR) kutoka Morogoro hadi Makutopora yenye umbali kilomita 336 za njia kuu na kilomita 86 za njia za kupishana treni na maeneo ya kupangia mabehewa jumla kilomita 422 kwa uzani wa tani 35 kwa ekseli.

 Kandarasi hii itakuwa na thamani ya jumla TZS Trilioni 4.3., mkataba umetiwa saini na Mtendaji Mkuu wa Rahco na TRL Nd Masanja Kadogosa na Mwanasheria wake Nd Petro Mnyeshi na kwa upande wa Yapi Merkezi waliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Bodi wake Bwana Erdem na Mkuu wa Miradi ya Ethiopia na Tanzania Bwana Abdullah .

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amesema utiaji sahihi wa kandarasi hii ya pili ni kuonesha dhamira isotetereka ya Serikali ya awamu ya 5 kuendeleza na kuimarisha miundo mbinu ya reli nchini kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya kiuchumi nchini.

Amesema reli ya kisasa ya SGR italeta mabadiliko makubwa sana kiuchumi na kijamii na maendeleo kwa jumla. Kwanza zitaokoa uharibifu wa barabara zilizojengwa kwa gharama kubwa. Bidhaa zinazosafirishwa kwa masafa marefu zitafika kwa gharama ndogo hivyo walaji watazinunua kwa bei nafuu.

Hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Ruaha katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(JKNICC) ilihudhuriwa na kaimu balozi wa Uturuki nchini pamoja na Wawakiishi wa Kampuni ya Yapi Markezi.

Wengine waliohudhuria ni Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano wakiongozwa na Katibu Mkuu wa WUUM -Uchukuzi Mhandisi Dk Leonard Chamuriho.

Mapema mwaka huu Februari 03, 2017, Yapi Merkezi na Mota Engil ya Ureno ziliingia mkataba na Rahco wa kujenga kipande cha kwanza cha reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro urefu wa jumla wa Kilomita 303. Ujenzi wa kipande hicho ulitiwa jiwe la msingi na Rais wa Tanzania Dk John Magufuli hapo Aprili 12, 2017 katika hafla kubwa ya aina yake iliyofanyika katika kituo cha Reli cha Pugu nje ya jiji la Dar es salaam.

Habari zaidi katika picha……

sgr 1 sgr2 sgr3 sgr4 sgr5 sgr6 sgr7 sgr8 sgr9 sgr10 sgr11 sgr12 sgr13 sgr14 sgr15 sgr16 sgr17 sgr18 sgr19 sgr20 sgr21 sgr22 sgr23 sgr24 sgr25 sgr27 sgr28 sgr29

 

sgr30prof na maez

Leave a Reply