WATATU WAFARIKI KATIKA AJALI YA TRENI NA BASI MOROGORO !

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI( PRESS RELEASE)
 
WATU WATATU WAFARIKI DUNIA KATIKA AJALI YA TRENI NA BASI MJINi MOROGORO!
 
Watu watatu wamefariki dunia jana saa 12:55 asubuhi katika ajali iliyohusisha basi dogo aina ya Nissan Civilian ilipo gonga treni katika makutano ya Tanesco Morogoro T438 ABR. Mmoja katika hao alifariki katika eneo la ajali ni mwanafunzi anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 6 ambaye bado hajatambuliwa wakati taarifa hii ikichapishwa.
 
Wengine wawili walipoteza maisha wakati wakipelekwa hospitali ya Mkoa wa Morogoro pamoja na majeruhi wengine 29. Marehemu wametambuliwa kuwa Asha Rashid Mtaalam(16) mwanafunzi wa Kidato cha 3 Sekondari ya Mji Mpya mkazi wa Kigurunyembe na mwingine Rajabu Rashid Kimanga(19) mwanafunzi wa Kidato cha 4 Sekondari ya Tushikamane..
 
Aidha imefahamika majeruhi 29 waliolazwa katika hospitali ya mkoa baadhi yao hali zao sio nzuri.
 
Dereva wa basi aliyesababisha ajali kwa kukaidi kutii amri ya kusimama kutoka kwa Watoa Ishara wa Kampuni ya Reli Tanzania amefahamika kuwa ni Charles Daimon (39) mkazi wa wa Kionda Maghorofani . Polisi wa Kikosi cha Reli wanafuatilia tukio hilo kwa lengo la kumfikisha mahakamani mtuhumiwa.
 
Wakati huo huo Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania umetuma Salaam za rambirambi kwa wafiwa wote waliopoteza watoto wao wapenzi katika ajali hiyo mbaya ya leo asubuhi.
Aidha wamewapa pole majeruhi wote 29 na kuwaombea wapate afueni ya haraka ili warejee katika shughuli zao za kujenga Taifa.Katika kuchangia gharama za mazishi TRL imetoa jumla ya Rambi TZS 2,000,000/= ambapo kila familia ya wafiwa watatu itapewa kila moja TZS Laki Tano na Laki Tano iliyobaki itasaidia gharama za matibabu kwa majeruhi wapatao 33 waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Jumla ya rambirambi hiyo itakabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe Regina Chonjo.ambaye ataratibu ugawaji wake kwa walengwa
 
Halikadhalika TRL imetoa wito kwa watumiaji wa barabara na hasa madereva kufuata na kutii sheria za barabarani ikiwa pamoja kuwa waangalifu wanapofikia makutano ya reli na barabara ili kuepuka maafa na uharibifu wa rasilimali chache tulizo nazo.
 
Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano ya TRL kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL ,
Ndugu Masanja Kadogosa,
Dar es Salaam,
Agosti 25, 2017 – Updated

Mhe Regina Chonjo DC wa Morogoro akipokea rambirambi za TRL TZS 2.000,000/= kutoka kwa Mhandisi Adolphina Ndyetabula.hii karibuni
Mhe Regina Chonjo DC wa Morogoro akipokea rambirambi za TRL TZS 2.000,000/= kutoka kwa Mhandisi Adolphina Ndyetabula.hii karibuni

trl ajali moro 3 WATATU WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI YA TRENI BASI MOROGORO! trl ajali moro 2

Leave a Reply