TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI(PRESS RELEASE)

Mkurugenzi Mtendaji wa TRL Nd Masanja Kadogosa

 

KADOGOSA ATEULIWA KUWA MKURUGENZI MTENDAJI MPYA WA TRL

 

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mnyaa Mbarawa amemteua Nd Masanja Kungu Kadogosa(41) kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni ya Reli Tanzania(TRL). Uteuzi huo umeanza Julai 01, 2016.

Ndugu Kadogosa mapema Februari 4, 2016 aliteuliwa na Serikali kukaimu nafasi hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL baada ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa awali Mhandisi Elias Mshana kuanza likizo ya kustaafu.

Aidha kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa juu katika TRL Nd Kadogosa alikuwa Mkurugenzi wa Mikopo katika Benki ya ya Maendeleo ya TIB. Kitaaluma Mkurugenzi huyo mpya ni msomi wa Masuala ya Uhasibu, Usimamizi wa Fedha  na Benki akiwa na Shahada ya Uzamili katika Utawala wa Biashara aliofuzu katika Chuo kikuu cha Umea mwaka 2004 nchini  Sweden .

 

Usafiri wa Treni ya Dar – Ubungo Maziwa waanza tena!

posted in: Emergency Notices, Notices | 0

Hatimaye huduma ya treni ya abiria ya Jijini Dar es Salaam maarufu kama ‘Treni ya Mwakyembe’ imeanza tena jana asubuhi Oktoba 22, 2015.

Kwa mujibu wa Idara ya Masoko ya TRL huduma hiyo imeweza kuanza kutokana na kuwasili ‘brake blocks’ za kutosha ambazo tayari zimefungwa katika mabehewa ya abiria ya treni hiyo.

Kuhusu uhakika wa huduma hiyo imefahamika hivi sasa TRL inatumia kichwa kikubwa cha treni aina  mpya vya Class 88U katika awamu mbili za asubuhi na jioni kila awamu ina safari 3.

Muda wa kuanza huduma ni saa 12 asubuhi kutokea kituo cha Ubungo wa Maziwa na saa 10 jioni kutokea Kituo cha Dar kwa siku za  Jumatatu hadi Ijumaa isipokuwa siku za Jumamosi na Jumapili na siku za sikukuu.

Atakayesoma taarifa hii amuarifu mwenziwe.

 

Imetolewa na Afisi ya Uhusiano kwa Niaba ya

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TRL

Mhandisi Elias Mshana.

Dar es Salaam,

Oktoba 23, 2015